![]() |
Mgunduzi wa taa, Thomas Edison alijaribu zaidi ya mara 1000 hadi akafanikiwa. |
Nikiwa mjini Dodoma, nakutana na mzee
Hamisi, yeye ni dereva wa taksi, na nilipomuuliza hii kazi anaifanya
tokea lini, ndipo akaniambia kuwa tokea mwaka 1996. Yaani hadi hivi
sasa ni kipindi cha miaka 18, na akaongeza kuwa anaendesha maisha kwa
mfumo huo hadi sasa, yaani kulipia ada za watoto, kujenga nyumba na
hata mahitaji ya kila siku sasa, wanakula na kwenda chooni kama
kawaida.
Hapo ndipo nikambukuka kijana mmoja
ambaye nilikutana naye mitaa ya Posta jijini Dar es Salaam, ambaye
yeye biashara yake ni kuuza madafu. Kama kawaida mpenda madafu mie
nikapiga breki ya miguu na kujipatia mawili (nimeyakosa kwa muda
mrefu aisee). Katika stori za hapa na pale, akaeleza kuwa anatumia
masaa 4 kwenda na kurudi kwa baiskeli hadi kuyafikisha mjini. Na siku
hiyo, anasema kwamba hakuwa na mengi, ila madafu 69 tu, ambayo
alianza kuuza mida ya saa saba mchana na kufikia saa tisa hakuwa na
kitu. Nikajifunza jambo, nikashukuru na kuishia.
Na kwa sasa namkumbuka kijana mmoja
mjini Same ambaye ni fundi viatu. Yeye ni habari ya kushona na
kung'arisha, benchi lake kaliweka kando ya ukuta na hana maneno na
mtu, anasubiria mtu aje – mwenye haja na kurekebisha lapa au kiatu,
chochote kinachovaliwa mguuni ambacho kitaleta mushkeli, basi yeye
yupo kurekebisha. Na yeye sikuacha kumuuliza mawili matatu, naye
akanieleza kuwa kabla ya kuanza siku, ni lazima aikabidhi mikononi
mwa BWANA, ili mambo yaende sawa – na kwa maelezo yake, hajawahi
kuangushwa na BWANA Mungu.
Sasa nirudi kwenye mada husika, mara
nyingi vijana mtaani na hata mjini wanaogopa kufanya jambo fulani kwa
maelezo kuwa ni jambo hilo ni gumu. Yaani kwamba hata wakifanya
watafeli, na hivyo kurudi nyuma, kwamba kuliko kufeli ni afadhali ya
kutofanya kabisa. Ndio hai vijana wapo, huenda hata wewe
umeshafikiria kufanya jambo fulani ukaogopa kufeli, na hivyo
ukaachana nalo.
Sasa basi nikukumbushe, kwa wale ambao
walibahatika kufika sekondari, wakati unamaliza darasa la saba, nina
hakika wengi waliambiwa kuwa kidato cha kwanza ni kigumu na sio
sehemu ya kufanya mchezo, huenda wengine waliacha shule kwa kusikia
hivyo, siok hata kujaribu, ila tu kwa kusikia. Na wewe uliyefanikiwa
kujitosa kuendelea, aidha klwa kulazimishwa ama kwa shauku ya kujua
ugumu wake ni nini, ama tu kwa vile ulishaelezwa kuwa elimu ni
ufunguo wa maisha, hakika ulifika na ukasoma kama kawaida, licha ya
kuhofia masomo ya kiingereza, sijui bunsen burner, mara sijui litmus
paper, ama bank reconciliation account, yote hayo uliyakuta na
kuvuka, na hatimaye kufika kidato cha tano na cha sita, huko nako ni
habari nyingine.
Lakini kwa huu mfano wa kuvuka darasa
la saba, ni dhahiri kwamba kma usingejaribu basi na usingefanikiwa.
Hata kufikia kidato cha nne, wengine hawakufanya mtihani, ila
waliofanya aidha walifeli ama kufaulu. Waliofaulu wakasonga mbele, na
waliofeli wakarudi kutafakari chanzo cha kuanguka na kisha kujipanga
upya kwa ajili ya kufanya mtihani wa taifa kwa mara nyingine.
Sasa basi, ni dhahiri kuwa ujinga
tulionao ndio unaotufanya tusisonge mbele kwenye mipango na mikakati
tuliyonayo maishani. Kwa mfano, unaogopa kuanza kozi unayotaka chuoni
kwa kuwa huamini kama utafanikiwa kuvuka.. ama unaogopa kuulizia hata
bei ya kiwanja kwa sababu unaamini huna hata hela,a achilia mbali
pesa.. pengine unaopoga kumuambia kuwa unampenda, ilhali anasubiria..
huenda unashindwa kuendelea kiuchumi kwa kuwa unaogopa kuweka genge
la matunda hapo nje.. ati matunda ni ya msimu, kwa hiyo watu
hawatakuja sana..
Kama Mzee Hamisi angeangalia idadi ya
taksi zilizopo barabarani, basi asingeingia kwenye biashara hizo,
kama huyu kijana muuza madafu angeangalia jasho litakalomtoka kwenda
na kurudi kila siku kufuata madafu hayo, basi angeachana na habari ya
shughuli hiyo kabisa, na labda tu nikuambie ameshakamatwa na mgambo
wa jiji kama leo, ila kesho akarudi palepale, amethubutu hadi
wakaelewa kuwa “huyu pia ni msakatonge, tuachane nae”. Na
kama fundi viatu angesema duka analoshabihiana nalo ni kubwa na lina
viatu vipya tu vilivyo bora, basi asingefungua eneo lake hilo.
Na wewe ukiangalia bodaboda zilivyo
nyingi barabarani ukasema usinunue kwamba haitakulipa, hiyo ni shauri
lako mwenyewe, ambalo niko kinyume nalo, ama ukisema kuna 'bajaj'
nyingi sana mjini na zinatosha kwa shughuli ya usafirishaji - kwamba
labda utafute kitu kingine, hayo ni mawazo yako mwenyewe, na huna
hata haja ya kumtafuta mchawi hapo.
Si unakumbuka, Lolote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako... kwenye Mhubiri 9:10 imeandikwa.
Sasa kama tatizo lako ni kusubiria 'memo' kutoka kwa Bwana mkubwa fulani
ili mambon yako yaende sawa, basi unaweza ukawa umejichangana vizuri
sana. Unamtegemea nani katika mambo yako? Wenzio wanarejea NENO, ya
kwamba Msaada wangu u katika BWANA aliyezifanya mbingu na nchi. Zaburi 121 imeandikwa.
Kama unaamini cheti chako kiko vizuri, lakini kila ukitoka nacho
kinarudi kama vile hakijapitiwa huko ulikokipeleka, basi ujue huu ndio
muda mzuri wa kumuambia Mungu, kwanini mambo yako tu yaende kombo?
Mwanzo mzuri ni kwa kuomba rehema, kutubu na kumtanguliza yeye katika
mambo yetu yote.
Hata unapotoka, ni watu wengi unakutana nao, wengine wenye mpango wa
kukuangusha ili mradi tu, na wengine hata sio watu kabisa, wanaonekana
tu wanatembea, kumbe wako katika ulimwengu tofauti kabisa.
Yafuatayo ni muhimu, kabla ya kutoka uikabidhi siku kwa BWANA Yesu;
Ukitoka uwe umeomba kibali kwake Yesu, maana akikukubali yeye, mwanadamu
ni nani apinge? Esta alipopata kibali kwa mfalme, hakuna aliyeweza
kumpinga wala kumfanya 'apotezewe', kila kitu kiliuwa sawa hata
kupelekea kuokolewa kwa kizazi cha Israel, huku mtesi wao, Hamani,
akiipata fresh Esta 7
Ni muhimu pia ukaomba mwongozo wake, kupitia Luka 21:15, amesema
atakupa kinywa na hekima ambayo watesi wako wote hawataweza kushindana
nayo wala kuipinga. Sawa sawia wale wote ambao unaona ni kikwazo kwenye
ofisi unayopeleka application yako, hebu omba kinywa na hekima - utapita
katikati yao.
Kwa machache haya (yanaweza kuwa mengi pia), chukua hatua na ufanye
jambo ambalo limekuwa likikutatiza, maana hauwezi ukaandika ripoti kama
hujafanya chochote, vivyo hivyo huwezi kuelezea changamoto kama
hujazipitia, jaribu sasa na ujue unatakiwa kufanya nini baada ya kufeli
mara ya kwanza. Ukianguka, sharti usimame na kuendelea na safari tena -
kama ambavyo mdunguzi wa balbu, mwanasayansi Thomas Edison alivyojaribu
zaidi ya mara 1,000 hadi ikaja kuwaka, na alipoulizwa na mwandishi wa
habari kwamba anajisikiaje kufeli mara elfu moja? Alijibu kuwa hajafeli,
bali ugunduzi huo umepitia hatua tofauti 1,000. Wewe umepitia hatua
ngapi hadi uchoke?
BWANA Yesu na akuwezeshe.
No comments:
Post a Comment