NENO LA MSINGI:
YAKOBO 3:2:
“Maana twajikwaa sisi sote pia
katika mambo mengi. MTU ASIYEJIKWAA KATIKA KUNENA, HUYO NI MTU
MKAMILIFU, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”
<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><
Viko vipimo kadhaa katika Biblia ambavyo tunaweza kujipima
ukamilifu wetu, huku tukijilinganisha na mfano wa mtu mkamilifu, Yesu
Kristo [ZABURI 37:37]. Kipimo kikubwa kimojawapo cha ukamilifu ni mtu
kuweza kuuzuia na kuutawala ulimi; na kuufanya useme yale tu ambayo Yesu
mwenyewe angeweza kuyasema. Biblia inasema kwamba, ulimi wa mtu asiye
mkamilifu ni ULIMI MOTO NA ULIMWENGU WA UOVU; nao ndio uutiao mwili wote
unajisi, na kuuwasha moto mfulizo wa maumbile [YAKOBO 3:6]. Ikiwa watu
wengi katika Kanisa la Nyumbani au Kanisa Kuu, ndimi zao ni moto na
ulimwengu wa uovu; basi mwili wote yaani Kanisa lote litatiwa unajisi na
kuwashwa moto kwa sababu yao. Moto wa ulimi unaweza kuligawanya
Kanisa, na kuleta makundi makundi kuondoa upendo kati yetu na kumfanya
Roho Mtakatifu awe mbali nasi. Biblia inasema “Ndugu zangu, haifai
mambo hayo kuwa hivyo[YAKOBO 3:10]. Biblia inazidi kutueleza kwamba,
mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu,
dini yake mtu huyo haifai na anajidanganya moyo wake kwamba ni mkristo
[YAKOBO 1:26]. Ikiwa tunataka kufahamika kwamba ni wakristo, basi
inatubidi tuwe na ndimi zilizo baridi, zinazotoa baraka wakati wote
katika Kanisa, na mataifa wanaotuzunguka.
Kwa sababu
hiyo, leo katika Kanisa la Nyumbani, tunapenda kujifunza tabia za ulimi
moto, ambao ni ulimwengu wa uovu. Kwa kuzifahamu tabia hizi za ulimi
moto, utaweza kujua ikiwa ulimi wako ni moto au la! Ikiwa ulimi wako ni
moto, basi hujakuwa mtu mkamilifu na Biblia inasema dini yako haifai
kitu na unajidanganya moyo wako. Inafaa basi, umwendee leo Yesu Kristo,
na kumwomba neema nyingi iliyoko katika damu yake iliyomwagika
msalabani; ili uweze kuuzuia ulimi wako kwa hatamu na kuufanya usiwe
moto tena, bali uwe baridi utoao baraka. Watu wote katika Kanisa la
Nyumbani na Kanisa Kuu, tukiwa na ndimi baridi zinazotoa baraka;
tutakuwa ni baraka kwa Kanisa lote la Mungu na Taifa lote, na Utatu wa
Mungu utafanya makao kwetu na kujidhihirisha kwetu kwa namna nyingi.
TABIA KUMI ZA ULIMI MOTO, ULIMWENGU WA UOVU:
1. HUSEMA UONGO NA KUSINGIZIA
Ikiwa
tunataka kufanya maskani yetu pamoja na BWANA, kusema uongo na
kusingizia; hakupaswi KAMWE kuonekana katika ndimi zetu [ZABURI 15:1-3a;
MITHALI 25:23; ZABURI 101:5a; ZABURI 101:6-7; MITHALI 19:5,9,22;
MITHALI 20:17; WAKOLOSAI 3:9; WAEFESO 4:25]. Ahadi zetu zinazotoka
katika ndimi zetu lazima ziwe kweli na amini. Tukimwambia mtu
tutakwenda kwake Jumatatu saa 10 jioni lazima iwe kweli hivyo hivyo,
isipokuwa tunapokuwa tumepata mambo mazito labda ugonjwa n.k. na hata
hapo tutatoa taarifa kabla za kuomba msamaha na kukiri kumkosea mtu
yule. Ndiyo yetu lazima iwe ni ndiyo na siyo yetu siyo. Kuvunja ahadi
ni kutokumjua Mungu [SOMA HOSEA 4:1-2; 2 WAKORINTHO 1:17-19]. Tunapotoa
ahadi na baadaye tunapogundua kuwa ahadi hiyo ni kwa hasara yetu, hata
hapo hatupaswi kuyabadili maneno yetu [ZABURI 15:1-2, 4]. Ikiwa hatuna
uhakika wa kufanya jambo, basi tusitoe ahadi. Sema kwa mfano “Nitakuja
kwako kesho kama nikiweza kumaliza shughuli zangu mapema. Hii ni ahadi
yenye masharti ya kutekelezwa kwanza. Ndugu asipokuona, basi atajua
kuwa masharti hayo hayakutekelezwa na hutakuwa umesema uongo. Mtu
asemaye uongo na kusingizia, mtu huyu ulimi wake ni moto.
2. HUFANYA MIZAHA AU UTANI
Katika
Ukristo, hakuna utani au mizaha. Hakuna watani katika wokovu. Utani
wa namna yoyote ni kinyume na Ukristo! Mtu wa kabila fulani utamsikia
akisema kuwa watu wa kabila fulani ni watani zake na utamsikia
akiwatania katika misiba na popote pale. Haya ni mambo ya mataifa au
watu ambao hawajaokoka. Ukristo hauna sehemu kabisa ya mizaha na utani.
Ulimi unaopenda mizaha au utani, ni ulimi moto, ulimwengu wa uovu
[SOMA ZABURI 1:1; MITHALI 26:18-19].
3. HUSENGENYA
Kusengenya
ni kumsema mtu vibaya kwa lengo la kumharibia sifa na kutaka aonekane
mbaya, hafai na wa kudharauliwa. Kusengenya hufanywa mtu akitajwa
wakati yeye hayupo katika mazungumzo hayo. Kusengenyana katika Biblia
ndiko kunakotajwa kwamba ni KUUMANA NA KULANA KUNAKOSABABISHA MAANGAMIZO
[SOMA WAGALATIA 5:15]. Kusengenyana huangamiza umoja na upendo katika
Kanisa na kusababisha makundi makundi. Mtu mwenye ulimi moto ndiye
ambaye hupenda kuwasengenya wenzie. Yeye ambaye anayemsengenya jirani
yake, hatakwenda kufanya maskani pamoja na Mungu [SOMA ZABURI 15:1, 3;
ZABURI 50:19-20, 22]. Wako wengine ambao hawasengenyi, lakini hupenda
kuyasikia masengenyo na kuyafurahia. Hawa pia hushiriki dhambi hiyo
sawa na wasengenyaji hao. Kusengenya lazima kuwe na sehemu mbili.
Anayesengenya na anayepokea masengenyo kwa kuyaruhusu masikio yake
kuyasikia na kuyafurahia. Kama hakuna wanaoyapokea masengenyo, basi
wasengenyaji watatoweshwa. Ni sawa na mtoa rushwa na mpokea rushwa.
Wote hatia yao ni ile ile. Mtu akizungumza na wewe na kumtaja mwingine
kwa sifa mbaya, mwambie pale pale mfanye maombi kwa ajili ya ndugu
anayetajwa, na mwambie aliyesema sifa hizo aombe mwenyewe.
4. HUSEMA MANENO YA DHARAU
Hatupaswi
kudharauliana sisi kwa sisi au kuwadharau mataifa. Yesu angetudharau
(maana tulikuwa wachafu na wasiofaa lolote), je, tungekuwa wapi leo?
Mtu mwenye ulimi moto, hujaa maneno ya dharau kwa wenzake. Amdharauye
mwenzake afanya dhambi [SOMA MITHALI 14:21a].
5. HUSEMA MANENO YA UKAIDI
Huutumia
ulimi wake kuwaambia wenzake kwamba hamjali Kiongozi, na kuwashawishi
wenzie wamuone Kiongozi wao mbaya na hafai. Huutumia ulimi wake kusema
hawezi kufuata maneno ya Mungu katika jambo fulani, na kuwashawishi
wengine kuasi. Mtu mwenye ulimi wa ukaidi kwa kiongozi wake wa Kanisa,
mume wake, boss wake kazini n.k. huyu ana ulimi moto. Ukaidi ni chukizo
kubwa kwa BWANA na ni ulimwengu wa uovu [SOMA MITHALI 3:32].
6. HUKASIRIKA NA KUTOA MANENO YA HASIRA
Mtu
mwenye ulimi moto, hukasirishwa na mambo madogo madogo tu na kuzira
kila kitu. Mtu wa jinsi hii hawezi kukaa na watu kwa amani. Wakati
wote yeye ni kununa tu na kutafuta ugomvi. Hasira ya namna hii siyo
sehemu ya ukristo. Hasira ya jinsi hii huzaa ugomvi na dhambi nyingi.
Hatupaswi kuiruhusu hasira kuutawala ulimi [MHUBIRI 7:9; MITHALI
22:24-25; WAKOLOSAI 3:7-8; YAKOBO 1:19-20]. Tunapaswa kumkasirikia
shetani tu anayewatesa na kuwatumikisha ndugu zetu katika dhambi, na
hasira yetu katika hilo, itatusukuma kuomba zaidi, kutoa mali zetu zaidi
na kuhubiri Injili zaidi kuikemea dhambi. Huku ndiko kuwa na hasira
bila kutenda dhambi [WAEFESO 4:26].
7. HUSEMA MANENO MENGI WAKATI WOTE
Mkristo
hazungumzi ili kuhakikisha ukimya unatoweka pale alipo! Kabla ya
mkristo kuzungumza, anayaangalia maneno atakayoyasema kwamba yatakuwa ya
kuwapa neema na kuwafaa wale watakaoyasikia [WAEFESO 4:29; WAKOLOSAI
4:6]. Mtu mwenye maneno mengi wakati wote, LAZIMA atakuwa ANAISHI
KATIKA DHAMBI. [SOMA MITHALI 10:19]. Katika maneno mengi wakati wote,
kunakuwa na kuongeza chumvi na kupamba ripoti au taarifa ili watu
wafurahi au wacheke, Kuongeza chumvi huku, ni kusema uongo na ni dhambi
iliyo mtego mkubwa kwa watu wengi wanaosema “Bwana Asifiwe”. Mtu mwenye
maneno mengi, wakati wote anapenda azungumze yeye tu, tena kwa sauti
kubwa ili asikiwe mbali, ulimi wake ni moto na ulimwengu wa uovu.
8. HUSEMA MANENO YA KIBURI NA MAJIVUNO
Mtu
mwenye ulimi moto, husema maneno ya kiburi na majivuno. “Pasipo mimi
kwaya haiwezi kuimba, lazima mnijali sana au siyo sitaimba”. “Kanisa
zima hakuna mwalimu kama mimi au anayeijua Biblia kama mimi”. “Kanisa
zima mimi ndiye msichana mzuri ninayeangaliwa na kutamaniwa na kila
mvulana”. “Nyumba yangu ni nzuri kuliko zote za kwenu”. “Nimesoma
kuliko kila mtu hapa”. “Hakuna mfanyakazi kama mimi kati yenu”.
“Hakuna mwombaji kama mimi, ninyi wote ni wavivu tu”. Maneno yoyote ya
kiburi na majivuno yanayofanana na haya siyo sehemu ya ukristo. Ulimo
moto hujivuna na kunena kwa kiburi. Kumcha BWANA, NI KUCHUKIA KIBURI NA
MAJIVUNO [SOMA MITHALI 8:13].
9. HUSEMA MANENO YA FITINA, UCHONGEZI, WIVU NA KUTETA KWA LUGHA YA KABILA WASIOIELEWA WANAOSIKIA
Ulimi
moto, hujaa wivu, fitina na uchongezi. Mtu mmoja mwenye ulimi moto
anapoutumia kunena maneno ya wivu, fitina na uchongezi, huweza kuliwasha
moto Kanisa la Nyumbani na hata Kanisa Kuu lote [SOMA 2 WAKORINTHO
12:20] Mkiwa wawili au watatu wa kabila fulani katikati ya wengine wa
kabila jingine, haiwapasi kutumia lugha ya kabila lenu kuzungumza na
kuwaacha wengineo hawaelewi lolote. Ni ulimi moto unaotenda hayo.
Ulimi baridi hujenga, kufariji, na kuwatia moyo watu wote, mahali pote;
na kuwafaa wahitaji wote. Siyo vibaya kusema lugha ya kabila lenu,
mnapokuwa ni ninyi peke yenu. Anapokuwepo asiye wa kabila lenu, semeni
Kiswahili ili yeye naye ajengwe.
10. HUHESABU MABAYA TU
Ulimi
baridi, wakati wote huhesabu mema ya mwenzie na kuyataja hayo wakati
wote. Ulimi baridi huyapuuza na kutokuyahesabu matendo mabaya
aliyoyatenda mtu ambaye alikwisha omba msamaha. Mtu mwenye ulimi moto,
humsema mwenzie na kumhesabia mabaya tu wakati wote kana kwamba hafanyi
jema hata moja. Mtu mwenye ulimi moto hamsifu mwenzake katika lolote
wala kutafakari mema aliyoyafanya, bali huorodhesha mabaya aliyoyafanya
mwenzie moja baada ya jingine. Ulimi wa upendo hauhesabu mabaya [1
WAKORINTHO 13:56]. Mtu mwenye ulimi baridi, anapowazungumza wenzie
wakati wote huyataja yale waliyoyafanya yenye sifa njema, yenye staha,
yenye wema, yenye sifa nzuri, yaliyo safi na ya haki na kuyatafakari
hayo [SOMA WAFILIPI 4:8].
Hizi ndizo tabia kumi za ulimi moto,
ulimwengu wa uovu. Itakuwa ni baraka ya ajabu Kanisa lote likiwa na
watu wenye ulimi baridi. Anza leo kuuzuia ulimi wako kwa hatamu katika
Jina la Yesu na kuufanya baridi. Ukimwomba Mungu, na kuchukua hatua,
hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Atakubadilisha leo na utakuwa na ndimi
wenye baraka na siyo ule unaolaani [SOMA YAKOBO 3:10-12]. Ukikizuia
kinywa chako na ulimi wako hivyo, utajilinda nafsi yako na taabu [SOMA
MITHALI 21:23].
M A S W A L I
(1) Kipimo kimojawapo cha mtu mkamilifu ni kipi? [YAKOBO 3:2]
—————————————————————————————————————-
(2) Mtu yupi ambaye Biblia inasema dini yake haifai kitu na anajidanganya moyo
wake? [YAKOBO 1:26]
—————————————————————————————————————-
—————————————————————————————————————-
Ikiwa watu wengi katika Kanisa watakuwa na ndimi ambazo ni moto, matokeo yake
yatakuwa nini?
—————————————————————————————————————-
(3) Taja tabia KUMI za ulimi moto, ulimwengu wa uovu:
(a)————————————————————————————————————-
(b)————————————————————————————————————-
(c)————————————————————————————————————-
(d)————————————————————————————————————-
(e)————————————————————————————————————-
(f)————————————————————————————————————–
(g)————————————————————————————————————-
(h)————————————————————————————————————-
(i)————————————————————————————————————–
(j)————————————————————————————————————–
4. Je unachukua hatua zipi kuanzia leo kuhakikisha unakuwa na ulimi baridi wakati wote
—————————————————————————————————————
—————————————————————————————————————
No comments:
Post a Comment