NENO LA MSINGI:
YAKOBO 3:2:
“Maana twajikwaa sisi sote pia
katika mambo mengi. MTU ASIYEJIKWAA KATIKA KUNENA, HUYO NI MTU
MKAMILIFU, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”
<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><
Viko vipimo kadhaa katika Biblia ambavyo tunaweza kujipima
ukamilifu wetu, huku tukijilinganisha na mfano wa mtu mkamilifu, Yesu
Kristo [ZABURI 37:37]. Kipimo kikubwa kimojawapo cha ukamilifu ni mtu
kuweza kuuzuia na kuutawala ulimi; na kuufanya useme yale tu ambayo Yesu
mwenyewe angeweza kuyasema. Biblia inasema kwamba, ulimi wa mtu asiye
mkamilifu ni ULIMI MOTO NA ULIMWENGU WA UOVU; nao ndio uutiao mwili wote
unajisi, na kuuwasha moto mfulizo wa maumbile [YAKOBO 3:6]. Ikiwa watu
wengi katika Kanisa la Nyumbani au Kanisa Kuu, ndimi zao ni moto na
ulimwengu wa uovu; basi mwili wote yaani Kanisa lote litatiwa unajisi na
kuwashwa moto kwa sababu yao. Moto wa ulimi unaweza kuligawanya
Kanisa, na kuleta makundi makundi kuondoa upendo kati yetu na kumfanya
Roho Mtakatifu awe mbali nasi. Biblia inasema “Ndugu zangu, haifai
mambo hayo kuwa hivyo[YAKOBO 3:10]. Biblia inazidi kutueleza kwamba,
mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu,
dini yake mtu huyo haifai na anajidanganya moyo wake kwamba ni mkristo
[YAKOBO 1:26]. Ikiwa tunataka kufahamika kwamba ni wakristo, basi
inatubidi tuwe na ndimi zilizo baridi, zinazotoa baraka wakati wote
katika Kanisa, na mataifa wanaotuzunguka.